MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chadema, Dk Willibrod Slaa jana alitoa tuhuma nzito dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa akisema kuwa taasisi hiyo imemuibia kura na hivyo hatayakubali matokeo ya uchaguzi wa urais.
Kauli hiyo imetolewa wakati Tume ya Uchaguzi (Nec) ikielekea kukamilisha kutangaza matokeo ya majimbo na kumtangaza mshindi, jambo ambalo litamfanya Dk Slaa na chama chake kuzuiwa na katiba ya nchi kupinga matokeo hayo mahakamani.
Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana akisema kuwa: "Kuna uchakachuaji mkubwa wa kura na kazi hiyo inafanywa na Usalama wa Taifa," alisema Dk Slaa ambaye matokeo yanayotangazwa na Nec yanaonyesha kuwa anaendelea kushika nafasi ya pili akiwa nyuma ya mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete.
Lakini Mwenyekiti wa Nec, Jaji Lewis Makame alipoulizwa kuhusu tamko hilo la Chadema, alimtaka Dk Slaa kuwasilisha taarifa zinazothibitisha madai aliyoyatoa kuwa Nec imekuwa ikitangaza matokeo yaliyochakachuliwa tofauti na zile alizopata.
Jaji Makame alisema kama madai ya Dk Slaa ni ya kweli, ni muhimu apeleke hizo idadi ya kura alizodai amepunjwa ili kuthibitisha madai yake dhidi ya tume hiyo.
Alisema idadi ya kura zinazotangazwa na Nec kwenye kinyang’anyiro cha urais ni zile ambazo wagombea hao wamezipata kihalali kwenye upigaji kura na wala hakuna upendeleo wowote.
“Mimi sijapata malalamiko yoyote kutoka kwa mgombea huyo, hivyo kama anayoyazungumza ni ya kweli kuna umuhimu wa kuthibitisha hiyo tofautu anayodai ipo, lakini kura tunazotangaza ni kura ambazo kila mgombea alizipata kwenye uchaguzi," alisema Jaji Makame
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la Karatu alionya kama Nec inaitakia mema nchi hii, ifute matokeo yote ya urais na uchaguzi urudiwe upya.
"Hatuwezi kukubali matokeo yanayopikwa na Usalama wa Taifa. Hayo si matakwa ya wananchi," alisema Dk Slaa baadaye kukaririwa kwenye TBC.
Kwa mujibu wa Dk Slaa, ambaye pia ni katibu mkuu wa Chadema, chama chake kimekuwa kikifuatilia kwa makini matokeo hayo na kugundua wizi mkubwa wa kura kwenye nafasi za urais na ubunge.
Mgombea huyo wa urais, ambaye mara nyingi hujenga hoja kwa kutumia ushahidi, alisema moja ya maeneo waliyogundua kuwepo kwa wizi wa kura ni matokeo ya Jimbo la Geita lililo mkoani Mwanza ambako alidai Nec ilitangaza kuwa kwenye uchaguzi wa rais, CCM imepata kura 17,792 na Chadema kura 3,789.
Lakini akasema kwa mujibu wa fomu walizonazo ambazo zilisainiwa na mawakala wao kwenye kata 20 za jimbo hilo, CCM ilipata kura 30,960 na Chadema 15,736.
"Nashangaa Nec wanatangaza matokeo haya kutoka wapi? Hayo ya Geita ni moja tu. Kule Hai, fomu zinaonyesha kwenye urais CCM ina kura 20,120 na Chadema 26,724, lakini Nec imetangaza kuwa CCM ina kura 35,910 na Chadema kura 18,513," alisema Dk Slaa huku akionyesha baadhi ya fomu kwa waandishi wa habari.
Dk Slaa pia alitoa mfano aliodai kuwa wizi wa kura katika kituo namba 00070103 cha Ubungo jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa fomu 24A inaonyesha CCM wamepata kura 68,727 na Chadema 65,450, lakini matokeo ya kata za Ubungo yanaonyesha CCM ina kura 70,472 na Chadema 72,252.
Dk Slaa alisema mbali na Ubungo, tatizo hilo pia alidai liko Kigoma Mjini ambako Chadema imeshinda kwa zaidi ya kura 500, lakini "matokeo yalichakachuliwa na kusababisha vurugu hadi askari wakawapiga mabomu wafuasi wa Chadema".
Pia alisema kwenye Jimbo la Segerea, ambako matokeo yalicheleweshwa kwa siku mbili na kutangazwa usiku wa manane juzi, mambo ni mabaya zaidi kwa kuwa fomu 21 A na B hazikuwepo na wasimamizi walikwenda nazo majumbani kulala.
"Kiwalani fomu hazikuwepo na matokeo hayakuonekana. Kipawa vituo vinne matokeo hayakuonekana na Vingunguti kuna vituo saba na Tabata vituo viwili ambako matokeo hayakuonekana," alisema Dk Slaa.